Ukraine kukagua msaada kutoka Urusi

Image caption Lori zilizoegeshwa karibu na mpaka wa Ukraine

Ukraine imesema kuwa maafisa wake wako tayari kukagua shehena iliyobebwa na masafara wa misaada kutoka Urusi.

Hapo jana waandishi wa habari walisema kuwa waliona msafara mdogo wa magari ukielekea maeneo ya kusini mwa Ukraine jambo ambalo lilikashifiwa sana na viongozi wa bara ulya.

Wakati huohuo Vifaru kadhaa vimeonekana vikielekea mpakani mwa Ukraine huku msafara wa magari ya msaada kutoka Urusi yakiegeshwa karibu na mpaka huo.

BBC iliona vifaru hivyo mapema ijumaa asubuhi lakini hakukuwa na hakikisho yalikuwa yakielekea Ukraine.

Wanahabari wengine wawili wanasema wameona magari ya jeshi ya Urusi yakiingia Ukraine.

Msururu huo wa magari bado unangoja ruhusa ili kuipeleka mizigo yake mijini ambayo imetekwa na waasi wanaounga mkono Urusi mashariki mwa Ukraine ambayo yamekumbwa na vurugu huku maafisa wa msalaba mwekundu wakiwa katika mji mkuu wa Ukraine kiev kwa ajili ya mazungumzo juu ya msururu huo.

Image caption Ukraine inasema kuwa ikotayari kukagua msafara wa msaada kutoka Urusi

Ukraine ambayo inahofia msururu huo unaweza kuwabebea waasi hao vifaa vya vita ilikuwa imetishia kuuzuia isipokuwa kama magari hayo yangekaguliwa moja kwa moja na maafisa wake .

Serikali ya Urusi imeendelea kukanusha kuwapa vifaa vya vita au hata mafunzo yoyote waasi hao ambao walitangaza niya ya kujitenga mwezi wa Aprili.

Mzozo huo ambao umepelekea kuuawa kwa watu zaidi ya 2000 umeongezeka wiki za hivi karibuni.

Msafara huo wa magari ambao ni wa kibinadamu ukiwa na takriban lori 260 uliendeshwa kwa saa tisa alhamisi kabla ya kuegeshwa kwenye uwanja mmoja karibu na mpaka.

Urusi imekanusha madai kwamba msafara wake ulikuwa ni singizio kutuma vifaa vya vita kwa waasi.

Image caption Magari ya kijeshi yalionekana yakiambatana na msafara wa msaada

Afisa wa msalaba mwekundu Laurent Corbaz akiwa Kiev ili kuzungumzia msafara huo alisema kwamba msalaba mwekundu ulikuwa na jukumu la kibinadamu pekee na kupelekwa kwa msaada huo hakufai kuhusishwa na siasa.

Msemaji wa msalaba mwekundu Anastasia Isyuk alisema msafara huo ulikuwa kusini mwa mji wa Kamensk-Shakhtinski na msalaba mwekundu ulikuwa katika mawasialiano na wasimamizi wa Urusi.

Aliongezea kusema kwamba hakukuwa na makubaliano yoyote kwenye mambo ya kuvuka mpaka na kibali cha forodha.

Steve Rosenberg ambaye amekuwa akiufuata msafara huo anasema kwamba swali muhimu sasa ni kile Urusi itafuatilia kufanya kama itaweza kupeleka msafara huo kuvuka mpaka kwa sababu itaonekana na mamlaka ya Ukraine kama uchochezi mkubwa kwa vile Ukrain itatuma msafara wake wa malori 75 ya msaada kwenda mashariki .

Marekani imeipa Urusi onyo ingine pia huku msemaji wa idra ya taifa Marie Harf akisema kwamba wamewaeleza warusi vizuri sana kwamba hawafai kuyapeleka malorri hayo ndani mwa Ukraine bila ya kutimiza matakwa yote ambayo serikali ya Ukraine ilitoa.

Wizara ya mambo ya kigeni ya Urusi imetaka kusitishwa kwa vita haraka alhamisi.

Rais wa Urusi Vladimir Putin alitembelea Crimea alhamisi ambayo Urusi ilimega kutoka Ukraine mwezi wa machi hatua ambayo iliibua lawama kutoka kwa mataifa ya bara Ulaya.