Kesi ya afisa wa jeshi Congo mtihani

Image caption Raia mashariki mwa DR Congo ndio waathirika wakubwa wa vita vya wenyewe kwa wenyewe

Umoja wa Mataifa umesema kesi ya vita vya uhalifu wa kivita katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo inayomkabili afisa wa zamani wa jeshi la nchi hiyo utakuwa mtihani kwa jeshi kutoa haki.

Luteni Kanali Bedi Mobuli Egangela anashitakiwa kwa makosa ya uhalifu yakiwemo mauaji, ubakaji na utesaji unaodaiwa kufanyika kati ya mwaka 2005-2006 mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo.

"Kesi kesi ya mfano," afisa wa Umoja wa Mataifa Scott Campbell ameiambia BBC.

Kamanda huyo wa zamani, akijulikana kama "Kanali 106", amekanusha mashitaka hayo.

Mgogoro mashariki mwa Congo umeendelea kwa muda mrefu baada ya kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo wakati vikundi vingi vyenye silaha vikishindana kudhibiti eneo lenye utajiri wa madini.

Kanali Egangela alikuwa kiongozi wa wanamgambo ambaye aliingizwa katika jeshi la kitaifa kama sehemu ya utekelezaji wa mpango wa amani, akiwa kamanda wa kikosi cha 106.

Ubakaji Mkubwa

Kabla hajajiunga na jeshi alituhumiwa kuwaandikisha askari watoto na kuamuru mashambulio katika vijiji kadhaa katika jimbo la Kivu Kusini na vitendo vya kuwadhalilisha raia vinasemekana viliendelea hata alipokuwa kamanda wa jeshi.

Baadaye kamanda huyo, mwaka 2007 alijiondoa katika ngazi za jeshi na kurejea kukiongoza kikundi chake cha wapiganaji waasi wa Mai Mai.

Shirika la Wanasheria Wasio na Mpaka, Avocats sans Frontieres limesema waathirika wapatao 100 wanatarajiwa kutoa ushahidi katika kesi inayomkabili kanali Egangela, japokuwa zaidi ya watu 900 wametambuliwa kuwa waathirika wa vitendo vinavyodaiwa kufanywa na wapiganaji wa kanali huyo.