Marekani yawashambulia wapiganaji Iraq

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Raia wa Yazidi walioachwa bila makao nchini Iraq

Idara ya Ulinzi nchini Marekani imesema kuwa mashambulizi ya ndege zisizo na rubani za Marekani yameharibu magari mawili ya wapiganaji karibu na mlima Sinjar kazkazini mwa Iraq.

Taarifa hiyo imesema kuwa mashambulizi hayo yanafuatia ripoti za mashambulizi yaliotekelezwa na wapiganaji wa Islamic State dhidi ya raia katika kijiji cha kawju.

Awali,maafisa wa kikurdi wamesema kuwa vikosi vya Islamic State viliwauawa wanachama 80 wa Yazidi katika kijiji hicho cha kazkazini mwa taifa hilo ijapokuwa haikuelezea iwapo kilikuwa kijiji cha Kawju.

Msemaji wa Islamic State amesema kuwa watu wa Yazidi wanaoishi katika maeneo wanayodhibiti wana uwezo wa kubadili dini, kuondoka ama kuuawa.