Watu 5 kortini kwa mauaji Uchina

Image caption Watu 5 wanaoshtumiwa kwa mauaji huko China wafikishwa mahakamani.

Watu watano waumini wa dhehebu lililopigwa marufuku nchini Uchina wamefikishwa mahakamani kujibu mashtaka ya kumpiga mwanamke mmoja hadi akafa.

Watano hao wafuasi wa dhehebu la ''Church of Almighty God'' walimvamia mama huyo katika mkahawa wa McDonalds katika mji wa Shandong ulioko mashariki mwa China.

Mama huyo Wu Shuoyan - alipigwa mbele ya mwanawe mwenye umri wa miaka 7 baada ya wafuasi wa dhehebu hilo kudai alikataa kupeana nambari yake ya simu ya mkononi kwa mmoja wa washiriki wa dini hiyo ambaye alitaka kumshawishi kujiunga na dini hiyo.

Mauaji ya Wu yaliwatamausha wachina ambao hawakuamini kuwa watu wangeweza kutekeleza mauaji mbele ya Umma.

Image caption Duka la Mcdonalds alikouawa Wu Shuoyan

Picha za kamera za siri zilionesha mashambulizi hayo mbele ya mwanawe na wateja wengine katika mkahawa huo ambao hawakufanya lolote kuokoa maisha ya mama huyo.

Wateja wa McDonalds walioshuhudia tukio hilo walidai kuwa walionywa wasiingilie kamwe tukio hilo la sivyo wembe utakuwa ni huohuo.

Dhehebu hilo linazaidi ya wafuasi milioni moja nchini humo licha ya kuwa limepigwa marufuku .

Mafundisho ya dhehebu hilo yanadai kuwa yesu Kristo alifufuka katika maumbili ya mwanamke wa Kichina.

Mamia ya wafuasi wa dhehebu hilo wamekamatwa nchini Uchina tangu mauaji ya Wu mwezi Mei.