Vikosi vya Iraq vyawakabili wapiganaji

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Kiwanda cha mafuta mjini Beiji Iraq.

Wanajeshi wa serikali ya Iraq wanasema kuwa wamelikabili shambulizi moja la wanamgambo katika kiwanda kikuu cha mafuta katika mji wa Beiji, na kuwaua wanamgambo kadhaa.

Kiwanda hicho kilichopo kazkazini mwa Iraq kimekuwa eneo la tukio la mapigano kadhaa kati ya vikosi vya serikali na wanamgambo katika kipindi cha miezi kadhaa iliopita.

Hapo jana msururu wa milipuko mitatu ya mabomu katika mji wa Kirkuk kazkazini mwa Iraq iliwauwa takriban watu 18.

Vyombo vya habari vya kikurdi vinasema kuwa miongoni mwa wale waliouawa ni maafisa wa kikosi cha kulinda amani cha kikurdi ,Peshemerga.

Image caption Islamic State

Kundi la wapiganaji wa kisunni Islamic State linashukiwa kutekeleza mashambulizi hayo.

Wapiganaji hao wa kikurdi waliuteka mji huo wenye utajiri wa mafuta mnamo mwezi Juni baada ya jeshi la Iraq kutoroka likihofia mashambulizi ya wapiganaji hao wa ki-sunni.

Wakati huohuo bomu jingine limelipuka katika mji wa Erbil,ambao ndio mji mkuu wa jimbo la wakurdi,ikiwa ni tukio la kushangaza kwa kuwa ndio eneo lenye utulivu nchini Iraq.

Awali mlipuaji wa kujitolea muhanga aliwaua takriban watu wanane mjini Baghdad karibu na makao makuu ya ujasusi.