Libya:Uwanja wa ndege wa Tripoli watekwa

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Uwanja wa ndege wa Tripoli

Muungano mmoja wa wanamgambo nchini Libya unasema kuwa umeuteka uwanja wa ndege wa kimataifa wa Tripoli baada ya mapigano makali kati yake na kundi pinzani la waasi.

Picha zilizowekwa katika mtandao zimeonyesha wapiganaji hao wakisherehekea juu ya ndege na katika majengo ya uwanja huo.

Muungano huo unaoshirikisha wanamgambo wa kiislamu pamoja na wanamgambo kutoka mji wa Misrata umesema kuwa uliuteka uwanja huo licha ya mashambulizi ya angani yanayodaiwa kutekelezwa na Misri pamoja na nchi za ufalme wa kiarabu.

Mwandishi wa BBC mjini Tripoli anasema kuwa kuna ripoti za kuendelea kwa vita kati ya makundi pinzani viungani mwa mji huo.

Uwanja huo umefungwa kwa takriban mwezi mmoja sasa kufuatia vita kati ya makundi pinzani ya wanamgambo yaliozuka tangu kuondolewa madarakani kwa aliyekuwa rais wa taifa hilo kanali Gaddafi mwaka 2011.