Vurugu za uchaguzi zaleta hasara Afghan.

Image caption Waziri wa Fedha wa Afghanistan Omar Zakhilwal

Waziri wa fedha nchini Afghanistan amesema vurugu kutokana na uchaguzi wa urais uliokumbwa na utata umepelekea hasara ya dola bilioni 5

Omar Zakhilwal aliieleza BBC kwamba ingebidi mishahara ya wafanyakazi wa serikali kupunguzwa, iwapo vurugu hizo hazitasitishwa kabla ya mwezi kuisha.

Uwekezaji kutoka mataifa ya nje ulikuwa umesimama na mapato ya serikali kupungua tangu kumalizika kwa zoezi la upigaji kura mwezi Aprili.

Wagombea wawili wamedai ushindi lakini mpaka sasa hakuna maelewano kuhusu kuunga serikali ya umoja wa kitaifa ingawa kura zinahesabiwa tena kwa usimamizi wa umoja wa kitaifa huku ikitarajiwa zoezi hili litachukua muda wa wiki mbili.

Viongozi hawa wawili wanaong'ang'ania madaraka, Ashraf Ghani na Abdullah Abdullah, wamekosa kuafikiana licha ya rais wa Marekani Barack Obama kuingilia kati.

Inasemekana vurugu hizi zinazidisha ughali wa maisha bei ya vyakula ikipanda na waasi wa Taliban wakichukua usukani kusini na mashariki mwa nchi.

Bwana Zakhilwal aliieleza BBC kwamba, walikuwa wamekomesha utumiaji wa fedha wowote usio wa maana jambo lilipelekea nchi kuzorota.

Ashraf Ghani, aliyeongoza kwenye matokea yasio rasmi alikuwa mwenye kupoteza zaidi kabla ya matokeo rasmi kutangazwa. Mpizani wake Abdullah Abdullah amelaumu wakuu wa uchaguzi kwa wizi wa kura huku wanaomuunga mkono wakiami ndiye aliyeshinda.