Spika ahusishwa na kashfa ya kuwauza watoto

Image caption Spika Hama Amadou alitoroka baada ya kuhusishwa na kashfa ya kuwauza watoto

Spika wa bunge la Niger ametoroka nchini humo baada ya kamati ya bunge hilo kuafikia kukamatwa kwake kuhusiana na kashfa ya kuwauza watoto.

Hama Amadou, ambaye tayari ameelezea azma yake ya kugombea urais mwaka 2016, anasema kuwa madai hayo dhidi yake yamechochewa kisiasa.

Mke wa pili wa spika huyo na watu wengine 16 walikamatwa mwezi Juni baada ya kutuhumiwa kuwauza watoto wachanga Kusini Mashariki mwa Nigeria.

Watoto hao huuzwa kwa maelfu ya dola kila mtoto.

Mwandishi wa BBC nchini Niger anasema kuwa kesi hiyo imetoa fursa tosha kwa chama tawala kumuondoa Bwana Amadou kutoka katika chama hicho tangu kukosana na muungano tawala.

Kashfa hii pia imewashtua wengi katika nchi hiyo yenye idadi kubwa ya waumini wa kiisilamu hasa kwa kuwa ni kosa kuonyesha kuwa watoto walioasiliwa na wako binafsi.

Imeripotiwa kuwa baadhi ya wanawake walidai walikuwa wajawazito na kwenda Nigeria kabla ya kurejea na watoto wao.

Kamati kuu ya bunge la taifa ambalo linamjumuisha naibu spika na wakuu wengine wa kamati nyinginezo, walikutana Jumatao, na kukubaliana kuwa polisi wanaweza kumkamata na kumhoji bwana Amadou kuhusiana na tuhuma hizo.

Wanasiasa sita wa upinzani walikataa kuhudhuria vikao hivyo ingawa idadi ya wabunge waliofika ilitosha kutoa uamuzi.

Kikao kamili cha bunge kitahitajika kufanyika ili kuondoa uwezekano wa bwana Amadou kushitakiwa.

Inadaiwa watoto 30 wameuzwa katika kashfa hii ambayo imehusisha kutengeza stakabadhi bandia na kubadili vyeti vya kuzaliwa vya watoto waliouzwa.