Waasi wabadili kauli kuhusu makubaliano

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Kwa mujibu wa makubaliano waliyofikia, Rais Kiir ataendelea kuwa Rais wa mpito

Waasi wa Sudan Kusini wamebadilisha kauli na kukataa makubaliano yaliyotiwa saini hivi karibuni ya kugawana madaraka na kumaliza ghasia za miezi kadhaa nchini humo.

Waasi hao wanasema makubaliano yaliyofikiwa na nchi wanachama wa IGAD, linamuidhinisha rais Salva Kiir aendelee kusalia madarakani katika kipindi kizima cha mpito.

Siku chache tuu baada ya kutia saini mkataba wa kubuni serikali ya mpito, upande wa waasi sasa unasema wapatanishi wanapendelea serikali.

Msemaji Taban Deng Gai, anasema hawahusiki kwa vyovyote katika makubaliano hayo ambayo yalitoa siku arobaine na tano kwa serikali na waasi kubuni serikali hiyo ya mpito itakayodumu miaka miwili unusu.

Kwa mujibu wa makubaliano hayo yaliyotiwa saini Ethiopia, Rais Kiir ataendelea kuhudumu kama rais nchini humo katika kipindi cha mpito wakati waasi watamchagua mgombea wa wadhifa wa waziri mkuu.

Waasi hao wamekashifiwa vikali kwa kuchelewesha mazungumzo na kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano.

Ripoti ya waangalizi wa IGAD inasema waasi wamekiuka makubaliano yote isipokuwa moja ya kusitisha mapigano. Pia wamekanusha madai kuhusika katika kudunguliwa kwa helikopta moja ya Umoja wa Mataifa katika mji wa Bentiu kwenye jimbo la utajiri wa mafuta la Unity.

Umoja wa mataifa na mashirika mengine ya misaada yameonya kuwa hali inaendelea kuzorota nchini Sudan kusini, huku taifa hilo sasa likikabiliwa na tishio la kiangazi