Pua la kielektroniki latambua maradhi

Kunusa haja kubwa kwa kutumia pua la kielektroniki, kunaweza kusaidia kutambua viini Bacteria vinavyosababisha maradhi mabaya.

Taarifa hii ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na watafiti nchini Uingereza.

Kifaa hicho kiliweza kunusa na kutambua viini tofauti kama vile 'Clostridium difficile' kutokana na kemikali zenye harufu mbaya ambazo zinatoka kwenye kinyesi.

Watafiti katika chuo kikuu cha Leicester wanasema kuwa matokeo ya utafiti wao yanaweza kusaidia katika kufanyia wagonjwa uchunguzi wa kimatibabu.

Pua la kielektroniki linafanyiwa utafiti ikiwa linaweza kugundua celi zenye Saratani kwa kuchunguza harufu inayotolewa na uvimbe kwenye Matiti na Mapafu.

Kadhalika pua hilo la kielektroniki linatumia kifaa ambacho kinaweza kupima kiwango kikubwa cha kemikali kila sekunde

Kila kemikali inayotambulika huwa ni ishara ya mafanikio kwa watafiti.

Mbali na kuweza kutambua viini ambavyo vinapatikana katika kinyesi na hata katika celi za saratani, watafiti wanaamini kuwa kuelewa muundo wa Bacteria inaweza kuwasidia kujua kwa nini baadhi ya viini vinasababisha maradhi wakati vingine havisababishi magonjwa.