Meya wa Italia amuandikia Yesu barua

Image caption Meya Giovanni Calabrese

Meya wa mji mmoja nchini Italia ameghadhabishwa mno na kile alichotaja kuwa uzembe na uvivu miongoni mwa wafanyikazi wa baraza lake la jiji.

Na ameamua kuchukua hatua anayoamini itawatia adabu.

Ameandika barua ya wazi ya malalamiko kwa Yesu Kristu. Amesema katika barua yake anaomba miujiza kutoka mbinguni kuwasaidia wafanyikazi hao na kuokoa mji wake.

Mji huo mdogo uitwao Locri uko chini kusini mwa pwani ya Uitaliano, wengine wakitania wakisema uko kidole gumba cha mguuni mwa uitaliano.

Kweli hautarajiwi kuwa na shughuli nyingi lakini meya wa mji huo Giovanni Calabrese asema kuna mipaka, imetosha,Uvivu umekithiri.

Katika barua yake anayosema amemwandikia Yesu Christo ili auokoe mji huo anataja matatizo mawili makuu.

Genge la mjini humo la kimafia na pili wengi wa wafanyakazi wa mji huo ambao amewataja kuwa ni wavivu .

Anafafanua kuwa ni wafanyakazi wachache mno ambao wanatekeleza kazi zao ipasavyo, waliosalia hukaa tu , wakiangalia, wakisubiri ujio wa hundi yao ya malipo ya mshahara ambao hamna kazi yoyote walioufanyia.

Mayor Giovanni anamlalamikia Yesu kuhusu hasa mahudhurio ya mashaka ya wafanyikazi hao - wengi wakiwa na tabia ya kutoa vijisababu vya kukosa kufika kazini.Hata baadhi yao kusingizia magojwa ya ghafla ili kukwepa zamu zao kazini.

Kisha barua hiyo yachukua mkondo wa kufoka, meya huyo akielezea jinsi alivyong'ang'ana angalau kurudisha huduma ya taa za barabarani zilizokuwa zimeharibika huku ndani ya maghala ya baraza hilo kukiwa na taa mpya yaani balbu zipatazo 15,000... Na mji unabaki kuwa kiza !

Barua ya Meya Giovanni haikuishia hapo amewatia pia lawamani polisi wa baraza hilo la mji wa Locri -kwamba wamezembea --- kwa maneno yake halisi anasema wamelala - kwa sababu wameshindwa kutoza faini madereva wasio na nidhamu barabarani ambako uendeshaji magari kiholela umeshamiri.

Hadi sasa hamna aliyetoa jibu lolote la hadharani kuhusu barua hiyo lakini ukitathmini hisia kali zilizojaa kwenye barua hiyo ya meya Giovanni huenda wakakosoa mtindo wake huo wa uongozaji wa baraza hilo.