Video ya kuchinjwa Sotloff ni hakika

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Steven Sotloff, mwandishi wa Marekani aliyeuawa kwa kuchinjwa na wapiganaji wa Islamic State.

Marekani imethibitisha kuwa picha ya video inayoonyesha kuchinjwa kwa mwandishi wa Marekani Steven Sotloff na wapiganaji wa Islamic State kuwa ina ukweli.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameyaita mauaji hayo kuwa ni "uhalifu unaostahili kudharaulika".

Serikali ya Uingereza imefanya kikao cha dharura cha kamati yake ya ulinzi na usalama baada ya vitisho vya kumuua raia wa Uingereza ambaye pia ameonyeshwa katika video hiyo.

Bwana Sotloff, mwenye umri wa miaka 31, alionyeshwa katika video mwezi uliopita ambayo ilimwonyesha mwandishi mwenzake wa Marekani James Foley aliyeuawa.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Rais Barack Obama

Bwana Sotloff alitekwa karibu na mji wa Aleppo kaskazini mwa Syria mwezi Agosti 2013.

Msemaji wa Baraza la Usalama la Taifa la Marekani, Caitlin Hayden amesema: "Jumuia ya Usalama ya Marekani imechambua picha za video zilizotolewa hivi karibuni zikimwonyesha raia wa Marekani na imefikia uamuzi wa kuzikubali kuwa ni za ukweli."

Msemaji wa familia ya Sotloff mapema alionyesha kuwa waliamini video hiyo kuwa ina ukweli wa kile kilichoonyeshwa na kutoa taarifa inayosema kuwa: "Familia inajua mkasa huu unaosikitisha na inaomboleza kibinafsi. Hapatakuwa na tamko la hadhara kutoka kwa familia wakati huu wa majonzi."

Kabla ya kuthibitisha mauaji hayo, msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Bi Jen Psaki alisema: "Iwapo video hii ni ya ukweli, tunasikitishwa na kitendo hiki cha kikatili, wakichukua maisha ya raia mwingine wa Marekani asiye na hatia. Mioyo yetu ipo pamoja na familia ya Sotloff."

Bi Psaki amesema inaaminika kuwa Wamarekani wengine "wachache"bado wanashikiliwa na wapiganaji wa Islamic State.

Awali Rais wa Marekani Barack Obama alisema kuwa Marekani haitatishwa na mauaji wa mwandishi mwingine wa habari Mmarekani na kundi la Islamic state.

Akiongea na waandishi wa habari nchini Astonia Rais Obama amesema kuwa mauaji hayo yanaichochea Marekani kukabiliana ziadi na magaidi.