Tisho la uhaba wa chakula S:Kusini

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Wanawake wanaponda na kusaga mbegu za maua ya Lily ili kuzipika

Mwandishi wa BBC Emmanuel Igunza ametembelea kijiji kimoja nchini Sudan Kusini ambapo watu wamelazimika kula mbegu na majani kutoka mtoni, huku kukiwa na tishio kubwa la baa la njaa.

Ni alfajiri katika kijiji cha Reke, makao ya takriban watui elfu tatu waliofurushwa makwao kufuatia mapigano kati ya wanajeshi wa serikali na bvikosi vya waasi katika jimbo la Unity lenye utajiri mkubwa wa mafuta

Mvua kubwa ilikuwa imenyesha usiku kutwa katika kijiji hicho kilicho kilomita 650 ( maili 400) Kaskazini Magharibi mwa mji mkuu wa Juba. Barabara hazipitiki ila tuu kutumia magari makubwa aina ya 'four-wheel.'

Watoto kadhaa wanacheza katika eneo moja la kijiji. Katika eneo linguine, kundi mmoja la wanawake linajenga nyumba ya muda, inayojulikana kama Tukul, wakitumia vijiti waliyokusanya kutoka mto uliokaribu.

Kwingineko, ajuza mmoja ameketi nje ya nyumba yake, inayofuka moshi kutoka ndani. Anatabasamu tunapomkaribia kisha anatoa kiko na kukiwasha, anaivuta na kutoa moshi huku akishangiliwa na baadhi ya majirani zake.

“ Sina chochote cha kufanya, maisha yangu ni magumu, lakini hilo halitanizuia kufurahia kiko chake,” ananiambia kupitia mkalimani.

Lakini tabasamu na vicheko hapa Reke vinaficha masaibu ya jamii hii.

'Wanakabiliwa na Njaa'

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Zaidi ya watu milioni 1.5 wametoroka makwao kutokana na vita

Wengi wao ni kutoka jamii ya Nuer, sawa na kiongozi wa waasi Riek Machar.

Rais Salva Kiir ambaye anatoka kabila la Dinka, amemshutumu kwa kutaka kupindua serikali mwezi Desemba.

Bwana Machar alikanusha madai hayo, lakini akakusanya kikosi cha waasi kupigana na Rais Kiir.

Zaidi ya watu milioni 1.5 wamefurushwa makwao kufuatia vita hivyo na Umoja wa Mataifa umeonya kuwa Sudan Kusini imo katika hatari ya kukabiliwa na baa kubwa la njaaKatika msimu huu wa mvua, barabara nyingi zimeharibika na hazipitiki.

Ni vigumu kupata au kusafirisha chakula.

Katika kijiji cha Reke, watu wanategemea chakula cha msaada kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula (WFP), lakini wanasema kupatikana kwake ni nadra sana.

"WFP imekuwa ikiwasaidia sana watu hapa Reke, lakini msaada huo huja mara moja kila baada ya miezi miwili.Ona jinsi watu hapa wana njaa," jamaa mmoja ananielezea

Wakaazi wa Reke sasa wanategemea magugu na mbegu wanayoyakusanya kutoka mto uliokaribu na hapa. Hukusanya mbegu hizo, na kuyasaga kisha huyapika kwa kuchanganya na maji.

Umoja wa Mataifa unasema takriban watu milioni nne wanakabiliwa na njaa baada ya wakulima kukosa kupanda katika msimu wa upanzi.

Wataalamu wameonya kuwa huenda Sudan Kusini ikakabiliwa na baa kubwa la njaa kufikia mwishoni mwa mwaka huu au mapema mwaka ujao.

Sudan Kusini ni taifa jipya zaidi duniani, na lilijitenga na kupata uhuru mwaka wa 2011, baada ya miongo kadhaa ya mapigano ya wenyewe kwa wenyewe na Upande wa kaskazini.

'Wanatembea kwa muda wa saa Sita'

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Watoto wengi wanakumbwa na utapia mlo kutokana na upungufu wa chakula

Kilomita chache kutoka Reke, tunafika katika kliniki moja inayowashugulikia watotot wanaougua utapya mlo.

Tangu mapigano kuzuka mwezi Disemba, kliniki hiyo inayoendeshwa na shirika la misaada la International Rescue Committee limekuwa likiwatibu watoto 16 kila wiki.

Lakini idadi hiyo imekuwa ikipungua, anasema muuguzi Peter Manyang.

"Hivi sasa kuna watoto sita waliolazwa hapa. Lakini hatujui iwapo ni hali inaimarika au ni kutokana na mvua kubwa inayonyesha na kuharibu barabara na hivyo kutatiza usafiri," Manyang ananieleza.

" Katika eneo hili, miundo msingi ni mbaya sana, hakuna barabara kutoka maeneo ya mashambani kuja katika eneo hili. Utapata kwamba kuna wale wanaotembea kwa zaidi ya saa sita kuja katika kliniki hiki.

Sio wote walioweza kufika, kuna akina mama walemavu, ambao hawakuweza, kwa hiyo ni wale tuu walio na nguvu waliotembea na kufika hapa. Anasema Manyang

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Shirika la mpango wa chakula duniani linafanya kila hali kuwafikishia watu chakula

Mojawapo ya watoto wanaotibiwa katika kliniki hii ni Stephen Nyamod mwenye umri wa mwaka moja.

Mama yake,Veronica Nyamod, alitembea kwa zaidi ya saa nne kumleta hapa wiki mbili zilizopita.

Licha ya matibabu ambayo amekuwa akipokea, afya yake haijaimarika. Madakitari wanasema uzani wake umepungua tena. Kwa sasa ana kilo 5 tuu. Miguu yake imekonda, na analia huku madaktari

wakimtibu. Mama yake mwenye umri wa miaka 33 anajaribu kumtuliza.

“ Kile ninachotaka tuu ni afya yake kuwa bora. Nina bahati nilifika katika kliniki hii. Hatukuwa na chakula cha kutosha katika kijiji chetu. Kuna watoto wengi wanaougua utapya mlo katika kijiji hicho, “ anasema

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Chakula hiki kwa magunia ndivyo ambavyo watu wengi hapa hupokea chakula cha msaada

Shirika la Umoja wa Mataifa la kushugulikia watoto UNICEF limeonya kuwa huenda zaidi ya watoto elfu hamsini wakafariki kufikia mwishoni mwa mwaka huu, iwapo hawatyapata msaada wa dharura.

Lakini kuna changamoto nyingi sana zinazokabili juhudi za kutoa chakula na misaada katika maeneo kama haya. Watu wengi wametoroka vita na sasa wanaisha katika vichaka na misitu. Wakati huohuo, mashirika ya misaada yamo mbioni kutoa maelfu ya tani za chakula na dawa kwa waliofuruishwa.

Na huku kukionekana kama hakuna suluhu au mwisho wa mapigano hayo, kuna hofu kuwa hali hii mbaya sasa itakuwa mbaya hata zaidi.

"Kuna changamoto nyingi sana hassa kuhusu usalama na pia barabara hazipitiki. Katika maeneo mengi, watu hawajapata msaada wowote tangu mapigano yalipozuka," anasema msemamji wa Unicef Sudan Kusini, Doune Porter.