Kenya yasaidia katika vita dhidi ya Ebola

Haki miliki ya picha afp
Image caption Rais Kenyatta asema msaada huo ni ishara ya umoja katika vita dhidi ya Ebola

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ameadhidi kutoa mchango wa dola milioni moja kwa mataifa ya Afrika Magharibi, Sierra Leone, Guinea na Liberia kuzisaidia kupambana na janga la Ebola ambalo limezitikisa nchi hizo.

Rais Kenyatta amesema kuwa mchango huo ni ishara ya umoja katika kuzisaidia nchi zilizoathirika na janga hilo kuweza kupambana nalo.

Hadi sasa nchi iliyoathirika zaidi kutokana na Ebola ni Liberia ambako maafisa kutoka shirika la madaktari wasio na mipaka wanasema kuwa wagonjwa wanalazimika kurejea nyumbani.

Hali hiyo inatokana na upungufu wa vifaa na shirika hilo kuzidiwa nguvu katika kuwasaidia waathiriwa. Inahofiwa kuwa Ebola inaendelea kuenea nchini humo kwa kasi ambayo ni vigumu kudhibiti.