Maeneo yaliyojitenga kupewa uhuru Ukraine

Image caption Rais Petro Poroshenko

Rais wa Ukraine Petro Poroshenkpo amesema kuwa atayapa uhuru zaidi maeneo yaliyoasi Mashariki mwa nchi lakini pia ameapa kuwa yatasalia kuwa chini ya utawala wa Ukraine.

Amesema kuwa usitishwaji wa mapigano kati ya vikosi vya serikali na makundi yaliyojitenga unaonekana kuwa mgumu kutekeleza kutokana na kile alichokiita kuwa uchokozi kutoka kwa magaidi.

Makundi hayo yameonyesha kupitia kwa video wakiuteka mji mwingine mashariki ya nchi wa Komsomolske.

Kadhalika Rais Poroshenko ameambia baraza la mawaziri kuwa vita vya kupigania uhuru wa Ukraine vingali vinaendelea , lakini tangu usitishwaji wa vita mashariki ya nchi, hali imebadilika pakubwa.

Aliongeza kuwa wakati wa kipindi hicho, majeshi ya Urusi yalisitisha harakati za kuendelea kuukaribia Ukraine , raia wengi wa Ukraine waliotekwa nyara waliachiliwa na waasi na mateka wengine wanatarajiwa kuachiliwa huru hivi karibuni.

Pia alisema kwamba ni vigumu kwa wakati huu kutekeleza mkataba wa amani Mashariki mwa Ukraine kwani wanajeshi wanaendelea kushambuliwa na waasi wanaotaka kujitenga na Ukraine.