Syria ilitumia Chlorine dhidi ya wakazi

Haki miliki ya picha ap
Image caption Shirika la OPCW linasema wakazi wameshambuliwa kwa gesi ya Chlorine

Gesi ya Chlorine ilitumika katika kuwashambulia watu Kaskazini mwa Syria mwaka huu, hii ni kwa mujibu wa shirika la kimataifa ambalo linanuia kuweka sheria zinazoharamisha silaha za kemikali.

Shirika hilo, (OPCW) linasema lina ushahidi kuonyesha kuwa gesi ya Chlorine ilitumika katika kuwashambulia wakazi .

Shambulizi lilifanyika mapema mwaka huu, katika vijiji vilivyo karibu na maeneo ambako waasi wamekuwa wakipigania na wanajeshi wa serikali.

Shirika la OPCW limekuwa likijihusisha na juhudi za kuharibu silaha za kemikali nchini Syria.

Mwaka mmoja uliopita, Syria ilitangaza kuharibu silaha za kemikali zilizokuwa zimewekwa nchini humo kuambatana na sheria za kimataifa.

Hata hivyo, Syria haikushurutishwa kutangaza kiwango cha silaha ilizonazo, ambazo zinaonekana kuwa za kemikali.

Ripoti hii ya hivi karibuni inasma kuwa kemikali za sumu zilitumiwa kuwashambulia watu vijijini hasa katika maeneo yaTalmanes, Al Tamanah na Kafr Zeta Kaskazini ya Syria.

Kadhalika ripoti hiyo inasema kuwa inaamini kwamba kemikali ya Chlorine ndiyo iliyotumika katika kuwashambulia wanakijiji.

Inasema wanajua kwamba ni gesi ya Chlorine iliyotumika kutokana na dalili walizokuwa nazo wanakijiji , walivyokuwa baada ya matibabu pamoja na maelezo kuhusu gesi hiyo.