Cameron afanya ziara ya 2 Scotland

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Cameron afanya ziara ya 2 Scotland kuwashawishi wasijitenge na Uingereza

Huku ikiwa zimebakia siku nne pekee kabla ya wakaazi wa Scotland kupiga kura ya maoni kuamua iwapo wataendelea kuwa sehemu ya Uingereza au la.

Waziri Mkuu David Cameron ameelekeza kampeni za kupinga kura hiyo Kaskazini mwa mpaka na Scotland kuwataka watu wasiunge mkono kutengwa kwa Scotland.

Ni ziara yake ya pili katika eneo hilo.

Katika hotuba anayotarajiwa kutoa, Bw. Cameroon anakabiliwa na kibarua kigumu cha kufafanua jinsi Scotland itakavyofaidika kifedha na kimahusiano endapo haitajitenga.

Vilevile, anatazamiwa kuwatahadharisha kuhusu kura hii ya maamuzi kuwa ikiwa itapita basi hakutakuwa na jingine ila kujitenga milele.

Wakati huo huo, aliyekuwa nahodha wa timu ya taifa ya kadanda ya Uingereza, David Beckham amewaomba wananchi kutounga kura hiyo ya maamuzi akisema kujitenga kwa Scotland hakufai na badala yake waangazie jinsi ya kuleta makubaliano mapya kati ya Scotland na UK.

Image caption Cameron afanya ziara ya 2 Scotland

Katika barua aliyoiyandika, aliwaomba wananchi kuungana na kupuuza masuala madogo madogo yanayowatenganisha.

Naye kiongozi wa wale wanaotaka kujitenga huko Scotland, Alex Salmond, amepuuzilia mbali ziara hiyo ya Bwana Cameron akisema kuwa Waziri Mkuu ameshikwa na wasiwasi.

Bwana Salmond alisema kuwa ana hakika kuwa watu wa Scotland watataka kujitenga kwa wingi wa kura kwa sababu kura hiyo hutokea mara moja baada ya muda mrefu.

Bw. Salmond anasisitiza ya kwamba kujitenga kwa Scotland kutoka kwa UK, kutasaidia pakubwa kukuza uchumi wa nchi hiyo mpya.

Wakati huohuo Malkia Elizabeth kwa mara ya kwanza amezungumzia kura hiyo ya maoni.

Ametoa wito kwa watakaopiga kura wafikirie sana juu ya siku za usoni za Scotland kabla ya kufanya hivyo.