Waraibu wa mihadarati watoroka matibabu

Image caption Kati ya watu 140,000 na 183,000 hutumia dawa za kulevya nchini Vietnam

Takriban watumiaji 400 wa dawa za kulevya wametoroka kutoka katika kituo cha waathiriwa wa dawa za kulevya Kaskazini ya Vietnam ambako walikuwa wanapokea matibabu kwa lazima.

Taarifa zinasema kuwa waraibu hao walivunja lango kuu la kituo hicho Jumapili na kutoroka.

Takriban watu 30 walirejea baadaye kwa hiari. Polisi kwa sasa wanawasaka waraibu waliosalia.

Mashirika ya kutetea haki za bindamau yamekuwa yakilaani hali duni ya vituo hivyo, vya kurekebishia tabia kwa waraibu wa dawa za kulevya.

Mwandishi wa BBC Nga Pham anasema kuwa nchini Vietnam, utumuaji wa dawa za kulevya ni tatizo kubwa sana katika jamii.

Waraibu wa dawa za kulevya hukamatwa na polisi mara kwa mara huku serikali ikiwalazimisha kwenda katika vituo vya kurekebishia tabia na kupokea matibabu.

Baadhi ya waathriwa pia hupelekwa katika vituo hivyo na jamaa wao.

'Sera nzuri zaidi'

Vyombo vya habari nchini humo vimesema kuwa waraibu hao walifanya uharibifu wa mali walipokuwa wanatoroka kutoka katika kituo hicho.

Hata hivyo baadhi ya maafisa wanasema kuwa waraibu hao walitoroka kwa lengo la kuishinikiza serikali kubadili sera ya kuwasaidia waathriwa wa dawa za kulevya.

Afisa mwingine, aliambia shirika la habari la AFP, kuwa kipindi cha matibabu kiliongezwa hadi miaka miwili au mitatu na kituo hicho pia kilipinguza kiwango cha pesa zinazotumiwa kwa chakula, hali ambayo imesababisha malalamiko kutoka kwa waraibu hao.

Hili ni tukio la pili la waraibu wa dawa za kulevya kutoroka kutoka kwenye kituo kama hiki katika mwongo mmoja.

Kwa mujibu wa ripoti watu 140,000 hadi 183,000 wanatumia dawa za kulevya nchini Vietnam.