''Naimarika zaidi Madrid'': Rodriguez

Haki miliki ya picha AP
Image caption James Rodriguez

Wakati Real Madrid leo wakitarajiwa kushuka dimbani dhidi ya Fc Basel James Rodriguez ambaye ni mshindi wa kiatu cha dhahabu katika kombe la dunia mwaka huu amesema kuwa anaendelea kuyazoea maisha ndani ya vijana hao wa Benabeu.

Mchezaji huyo raia wa Colombia aliyejiunga na timu hiyo akitokea klabu ya Monaco, Ufaransa kwa kitita cha pound million 71 ameweza kuwapa matumaini baadhi ya mashabiki kwamba huenda akaendelea kufanya vyema ndani ya klabu hiyo pia.

Ari ya mchezaji kufanya vizuri imeonekana bayana kama alivyokaririwa akieleze nia yake ya ndani kufanya vyema,'kila siku nazidi kuimarika kimwili na kiakili''ameeleza mshambuliaji huyo.

Rodriguez mwenye umri wa miaka 23, amekuwa ni sehemu ya madrid timu ambayo imeshapoteza mechi zake tatu za mwanzo katika ligi ya Hispania na kuifanya timu hiyo kushika nafasi ya 12 katika msimamo wa ligi hiyo.