Sudan kusini yaepuka baa la njaa

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Jamii ambazo hazikuathirika na mapigano Sudan Kusini zilipanda vyakula

Sudan Kusini imeepuka baa la njaa lakini ukosefu wa chakula wasalia kuwa swala nyeti hasa mwakani.

Weledi wa masuala ya mlo wameonya kwamba watu wengi wataathirika na njaa endapo hatua za dharura hazitachukuliwa mara moja kuchanga fedha na kusambaza vyakula nchini humo.

Ripoti ambayo imetolewa hivi punde na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali nchini Sudan Kusini inasema kuwa ingawa hali ya chakula imeanza kuimarika hasa msimu huu wa mavuno, kuendelea kwa vita kumemaanisha sekta ya kilimo iliathirika na hali ilivyo sasa ni mbaya zaidi ikilinganishwa na miaka mingine.

Maeneo ambayo hayajashuhudia vita yamechangia kuzalisha chakula nchini humo.

Licha ya hayo, imekadiriwa kuwa watu milioni moja u nusu wanakumbwa na ukosefu wa chakula.

Idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka maradufu ifikapo mwaka ujao endapo hatua za dharura hazitachukuliwa kukabiliana na utapia mlo na njaa.

Ripoti hiyo imetolewa na mashirika 14 yanayofanya kazi nchini Sudan Kusini yakiwa pamoja na Umoja wa Mataifa.