Kenyatta asita kwenda kikao ICC

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Kesi dhidi ya Rais Kenyatta bado haijaanza kusikilizwa

Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta,amesema kuwa hawezi kuhudhuria kikao alichoagizwa kuhudhuria na mahakama ya kimataifa ya ICC mwezi ujao kutokana na kazi nyingi aliyonayo.

Mahakama hiyo ilimtaka afike mbele yake kujibu madai kuwa serikali yake imekataa kuwasilisha shatakabadhi zinazohitajika na mahakama hiyo katika kesi inayomkabili.

Kenyatta kupitia kwa mawakili wake ameitaka mahakama ya ICC kuahirisha kikao hicho.

Alikuwa ameamrishwa kufika mbele ya kikao hicho cha siku mbili baada ya upande wa mashitaka kulalamika kuwa rais huyo amekataa kuwasilisha ushahidi mbele ya makahama hiyo.

Hata hivyo mawakili wa rais Kenyatta wameitaka mahakama hiyo sasa kumruhusu mteja wao imma ashiriki kikao hicho kupitia video ama skype, au wao wajibu masuali kwa niaba yake.

Rais Kenyatta amesema kuwa yeye yuko na shughulio n yingi sana kuweza kuhudhuria kikao hicho mwezi ujao.

Amesema kuwa mikutano miwili muhimu ya kiserikali ilikuwa imeshapangwa kufanyika nchini Uganda katika tarehe hizo wanazoitisha mahakama.

Rais huyo na naibu wake William Ruto wanakabiliwa na mashtaka ya kupanga mauaji ya kikabila wakati wa machafuko yaliyozuka nchini Kenya baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2007.

Kesi hiyo tayari imechelewehwa kwa muda mrefu huku mashahidi wakuu wakijiondoa na pia kumekuwa na malalamiko kuwa baadhi ya mashahidi hao wame tolewa vitisho kubadilisha ushahidi wao au kuondoa kabisa.

Mwendesha mashtaka mkuu Fatou Bensouda na na mawakili wa waathiriwa wamesalia na siku tatu sasa kujibu ombi hilo la Rais Kenyatta la kuahhirisha kikao hicho.

Mawakili wa rais Kenyatta wame kuwa wakisisitiza kila mara kuwa kesi hhiyo iondolewe kabisa kutokana na kile wanachodai kuwa ukosefu wa ushahidi dhidi yake.

Hakuna aliye shitakiwa hadi leo nchini Kenya kwa kuhusika na kupanga machafuko hayo yaliyoizonga Kenya mwishoni mwa mwaka wa 2007