Ebola yadhibitiwa Nigeria na Senegal

Haki miliki ya picha AP
Image caption Taasisi ya kuthibiti magonjwa nchini Marekani CDC

Virusi vya ugonjwa wa Ebola huenda vimedhibitiwa nchini Nigeria na Senegal,kulingana na maafisa wa afya nchini Marekani,baada ya visa vipya kutoripotiwa katika mataifa hayo kwa kipindi cha mwezi mmoja sasa.

Taasisi ya kudhibiti magonjwa nchini Marekani CDC imesema kuwa mlipuko wa ugonjwa huo unaweza kutangazwa kwamba umeisha nchini Nigeria ifikiapo mwezi ujao.

Hatahivyo ugonjwa huo unaendelea kuathiri maisha ya raia wengi katika maeneo mengine ya Afrika Magharibi hususan Liberia,Guinea na Sierra Leone.

Shirika la afya duniani WHO linasema kuwa zaidi ya watu 3000 wamefariki kutokana na ugonjwa huo kufikia sasa wengi wakitoka nchini Liberia.

Mlipuko huo ndio hatari zaidi kuwahi kutokea katika historia ya ugonjwa huo.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Afisa wa CDC Tom Frieden

Mkuu wa Umoja wa Mataifa anayesimamia kitengo cha kukabiliana na ugonjwa huo amesema kuwa hatua kubwa zitapigwa katika kipindi cha siku sitini zijazo kuuthibiti ugonjwa huo.

Mlipuko wa ugonjwa huo katika mataifa ya Nigeria na Senegal umekuwa mdogo ikilinganishwa na mataifa mengine ya Afrika Magharibi huku visa 20 vikithibitishwa kwa jumla kati ya mataifa hayo mawili.

Nchini Nigeria ,ambalo ndio taifa lenye idadi kubwa ya watu barani Afrika,kumekuwa na visa 19 vya ugonjwa huo ambavyo vimethibitishwa pamoja na vifo vinane tangu kisa cha kwanza kugunduliwa mnamo mwezi Julai.

Kisa cha mwisho kuripotiwa nchini humo kilikuwa kile cha tarehe 5 mwezi Septemba kulinga na CDC.