Al-Shabaab wapata pigo Somalia

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Wapiganaji wa kundi la Al-Shabaab

Wanajeshi nchini Somali wameidhibiti milima ya Galgala kutoka kwa wapiganaji wa kundi la Al-Shabaab,kulingana na utawala wa eneo hilo.

Wanamgambo hao walikuwa wakiidhibiti milima hiyo ya Kaskazini mwa taifa hilo kwa miaka kadhaa.

Waziri wa habari wa Puntland amesema kuwa kamanda wa Alshabaab katika eneo hilo alisalimu amri miezi minne iliopita.

Kundi hilo linaloshirikiana na lile la Al-Qaeda lina makao yake makuu kusini na katikati mwa somalia ambapo vikosi vya Umoja wa Afrika vinafanya mashambulizi.

Abdiweli Hirsi Abdille,ambaye ni waziri wa habari wa jimbo la kaskazini mashariki mwa Somalia Puntland amesema kuwa vikosi vya serikali vimeliteka jimbo hilo la Glagala katika mashambulizi yaliotekelezwa alfajiri.

Hatahivyo hakutoa maelezo yoyote kuhusu wafungwa ama waliojeruhiwa.

Lakini kituo cha redio cha Al Furqan,kinachojulikana kwa kuwapendelea wapiganaji wa Al-Shabaab kimeripoti kwamba magari mawili ya kijeshi yaliharibiwa na wanajeshi 16 kuuawa.

Galgala ni eneo la kipekee la Puntland ambalo limekuwa chini ya udhibiti wa Alshabaab.

Kamanda wa Al-Shabaab katika eneo hilo Said Atom alijiunga na vikosi vya serikali mwaka huu na kuwawacha wapiganaji wake katika jimbo la Puntland.

Wapiganaji wa Al-Shabaab wamefurushwa kutoka miji mikuu katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni ,lakini bado wanadhibiti miji midogo katika maeneo ya mashambani.