Wenger: Welbeck ana kasi ya umeme

Haki miliki ya picha PA
Image caption Danny Welbeck

Mkufunzi wa kilabu ya Arsenal nchini Uingereza Arsene Wenger amemtaja mshambuliaji wake Danny Welbeck kama mchezaji mwenye kasi ya 'umeme' baada ya kuifungia timu ya Arsenal mabao matatu siku ya jumatano katika mechi ya kilabu bingwa barani Ulaya dhidi ya Galatasaray.

Mshambuliaji huyo wa Uingereza mwenye miaka 23 alifunga mabao mawili katika kipindi cha kwanza katika uga wa Emirates kabla ya kupata bao lake la tatu katika kipindi cha pili.

Welbeck sasa amefunga mabao manne katika mechi tatu na Kocha Wenger amesema kuwa alidhani mchezaji huyo ana kasi lakini sasa amebaini kwamba ana kasi ya umeme.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Arsene Wenger

Amesema kuwa ana matumaini kwamba mabao hayo matatu yatampa motisha zaidi.

Danny Welbeck sasa ni mchezaji wa sita nchini Uingereza kufunga mabao matatu katika mechi moja ya kombe la kilabu bingwa barani Ulaya.

Welbeck alicheza kama mshambuliaji mkuu dhidi ya Galatasaray ,huku Alex Sanchez,Mesut Ozil na Alex Oxlade-Chamaberlain wakiwa nyuma yake.

Wanne hao walishirikiana vyema,huku Welbeck akionekana kufanya mashambulizi makali baada ya kupata pasi murua kutoka kwa Sanchez na Oxlade Chamberlain.