IS yadhitibi maeneo matatu Syria

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Islamic state

Wapiganaji wa Islamic State (IS) wameingia katika mji muhimu wa Kobane ulio mpakani mwa Syria na Uturuki na kutwaa udhibiti wa maeneo matatu baada ya mapigano ya mtaa kwa mtaa na walinzi wa Kikurd wa Syria.

Wapiganaji wa IS waliingia wilaya za mashariki mwa Syria Jumatatu, wakipeperusha bendera yao nyeusi katika majengo na vilima.

Maafisa wa eneo hilo wanasema raia wapatao 2,000 wamekimbilia katika mpaka wa Uturuki.

Kuutwaa mji wa Kobane, uliokuwa umezingirwa kwa wiki tatu, utawapa IS udhibiti wa mpaka wa Syria na Uturuki.

Zaidi ya raia 160,000 wa Syria wengi wao wakiwa ni Wakurd, wameukimbia mji huo. Mapema afisa kutoka eneo la Kobane, Idriss Nassan, ameiambia BBC kwamba mji huo ni "dhahiri utaanguka karibuni".

Amethibitisha kuwa IS kwa sasa wanadhibiti Mistenur, kilima cha mkakati katika mji wa Kobane na kwamba kuna mapigano makali. Kobane kwa sasa umezingirwa pande tatu.

Karwan Zebari, mwakilishi wa serikali ya Wakurd katika eneo hilo nchini Marekani, ameiambia BBC kuwa itakuwa hali mbaya iwapo IS itachukua udhibiti wa mji wa Kobane.

"Kama hali hii itaendelea, kama hakuna msaada wa kimataifa, msaada wa kijeshi kufika kwa ajili ya wakaazi wa Kobane na hawa wapiganaji wa Kikurd wanaopigana Kobane, mji huu utaangukia mikononi mwa IS," amesema

Ameiomba Uturuki kuchukua hatua ya kuwasaidia wakaazi wa Kobane.