Vita dhidi ya IS vyachacha mjini Kobane

Haki miliki ya picha AFP
Image caption wapiganaji wa Islamic State

Wapiganaji wa Kikurdi wanakabiliana vikali na wanamgambo wa Islamic State katika mji wa mpakani mwa Syria Kobane,huku mashambulizi dhidi ya wanamgambo hao yanayoongozwa na Marekani yakiendelea.

Mwandishi wa BBC anayeshuhudia vita hivyo amesema kuwa mashambulizi kadhaa yamefanyika pamoja na milipuko ya gurunedi.

Katika ripoti ya hivi karibuni,makao makuu ya majeshi ya Marekani yamesema kuwa mashambulizi sita ya angani yameharibu vifaa vya kijeshi vya kundi la Islamic State katika eneo la Kobane.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption kobane

Mjumbe wa Umoja wa mataifa nchini Syria ametoa wito kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua ili kuwazuia wapiganaji wa Islamic state kuuteka mji huo muhimu.

Steffan de Mistura ameiambia BBC kwamba kutekwa kwa mji wa Kobane kutasababisha mauaji na janga la kibinaadamu.

Utekaji wa mji wa Kobane utawapa wapiganaji wa Islamic State udhibiti wa eneo kubwa la mpaka wa Syria na Uturuki,ambao umekuwa ukitumika kama njia ya wapiganaji wa kigeni wanaoingia nchini Syria pamoja na kuwasaidia wapiganaji hao kusafirisha mafuta kutoka maeneo inayodhibiti.

Vita vya wiki tatu kuwania udhibiti wa mji wa Kobane vimesababisha mauaji ya watu 400,huku zaidi ya raia 160,000 wa Syria wakilazimika kukimbilia nchini Uturuki.