Mtandao wa Twitter waishtaki Marekani

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Twitter

Mtandao wa Twitter umeishtaki serikali ya Marekani kutokana na sheria zake za ujasusi.

Kulingana na sheria za sasa, mtandao wa Twitter hauwezi kutoa habari fulani kuhusiana na ombi la serikali ya Marekani kutaka kupewa data za wanaotumia mtandao huo kwa sababu za kiusalama.

Twitter Inadai kwamba hatua hiyo inakiuka uhuru wa kujieleza kama inavyoelezwa katika marekebisho ya kwanza ya katiba ya Marekani.

Kampuni hiyo iliwasilisha kesi hiyo mahakamani katika juhudi za kuilazimisha serikali kuwa wazi kuhusu ombi lake la data za watu binafsi.

''Tunaamini kwamba tuna haki chini ya kifungu cha kwanza cha mabadiliko ya kikatiba kujibu mahitaji ya wateja wetu mbali na taarifa ya serikali ya Marekani kwa kutoa habari kuhusu ujasusi wa serikali ya Marekani'',wakili wa Twitter Ben Lee aliandika katika blogi..

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Obama

Twitter iliishtaki idara ya haki ya Marekani na ile ya ujasusi katika mahakama moja ya Carlifornia siku ya jumanne.

Mnamo mwezi Aprili,Twitter ilitoa ripoti ya uwazi kwa serikali ya Marekani ili kuchapishwa;lakini kufikia sasa maafisa wa marekani wamekataa ombi la mtandao huo kutoa ripoti hiyo kwa uma.

Ripoti hiyo inashirikisha habari fulani kuhusu uhalisi na idadi ya maombi kuhusu watumizi wa mtandao wa Twitter yanayohusiana na usalama wa taifa hilo.