Vurugu zaanza upya nchini CAR

Image caption Inaarifiwa makabiliano yameanza kati ya wakristo na waisilamu

Taarifa za hivi punde kutoka katika Jamuhuri ya Afrika ya Kati, zimeripoti kusikika kwa milio ya risasi na mashambulizi makali katika mji mkuu Bangui.

Watu watano wanasemekana kufariki katika makabiliano kati ya wakristo na waisilamu ambayo inaarifiwa yalianza Jumanne.

Pia kuna taarifa za watu wengine kujeruhiwa.

Kamati ya kimataifa ya msalaba mwekundu, inasema kuwa nyumba na biashara za watu zimeharibiwa baada ya kuporwa na kisha kuteketezwa.

Duru zinasema kwamba ghasia za sasa hivi ndio mbaya zaidi kushuhudiwa mjini Bangui tangu vikosi vya Umoja wa Mataifa kuanza kushika doria nchini humo mwezi jana.

Zaidi ya watu elfu tano wamefariki tangu vurugu kuzuka kufuatia makabiliano ya kikabila mwishoni mwa mwaka jana.