Ebola:Mshambuliaji wa Guinea ajiondoa

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Alhassane Bangoura

Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Guinea Alhassane Bangoura amefichua kwamba alijiondoa katika kikosi kitakachokabiliana na timu ya taifa ya Ghana kwa sababu mchezaji mwenzake wa timu ya Rayo Vallecano alihofia kwamba huenda akaambukizwa ugonjwa wa Ebola.

Mamia ya watu tayari wamepoteza maisha yao kutokana na virusi vya ugonjwa wa Ebola nchini Guinea hivyo basi taifa hilo limechukua hatua ya kuihamisha mechi yao ya kufuzu kwa kombe la taifa bingwa barani Afrika nchini Morocco hapo jumamosi.

"Nilimuomba mkufunzi wa timu ya taifa ya Guinea Michel Dussuyer kuniruhusu nijiondoe kwa sababu wenzangu waliogopa kwenda,'' Bangoura aliiuambia mtandao wa Rayo.

''Rayo haikuniambia chochote, maamuzi haya ni yangu binafsi''.

Mkurupuko wa Ebola unaoshuhudiwa kwa sasa ktika eneo la Afrika Magharibi umewaua watu wengi zaidi kuliko magonjwa mengine yote kwa pamoja, huku mataifa ya Guinea, Sierra Leone na Liberia yakiathirika zaidi.

''Nina huzuni sana kwamba sitaweza kushiriki mechi hiyo.Nitazungumza na wachezaji wezangu nisikie kauli zao''

Kama njia moja ya kuzuia kuenea kwa virusi vya Ebola, shirikisho la kadanda nchini Sierra Leone lilisitisha mechi zote za kadanda kufanyika.

Pia shirikisho la kadanda la bara Afrika (CAF) liliamuru mechi zote zinazohusisha timu za Sierra Leone, Guinea na Liberia zilizoratibiwa kuchezewa katika nchi hizo kuhamishwa katika nchi nyingine tofauti

Sierra Leone tayari imepata mataifa yatakayowaruhusu kuandaa mechi zake na wamewahakikishia kwamba wameweka mikakati kabambe ya kuhakikisha ugonjwa huo hauambukizwi wachezaji na wakufunzi.