Ebola:Hofu ya maambukizi zaidi

Haki miliki ya picha AP
Image caption Kutokana na kasi ya kuenea kwa Ebola mataifa yamechukua hatua za kuwachunguza watu

Shirika la afya duniani limetahadharisha kuwa linatarajia kuona maambukizi zaidi ya Ebola licha ya kile linachosema ni kuongeza kasi juhudi za kupambana na janga hilo katika wiki chache zilizopita.

Msemaji wa shirika hilo, Daktari, Chris Dye, anasema kuwa wagonjwa katika maeneo yaliyoathirika zaidi ,Guinea, Sierra Leone na Liberia kuna uhaba wa vitanda

Mojawapo ya mashirika yanayoongoza vita dhidi ya ebola huko Afrika magharibi limesema ulimwengu hauna budi kuchapuza harakati za kuzuia janga hilo.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Mgonjwa aliyeambukizwa ugonjwa huo nchini Marekani alifariki

Rais wa shirika hilo Medecins sans Frontieres, Joanne Liu, amesema haelewi kwanini miezi 7 baada ya kugunduliwa kwa maambukizi ya ugonjwa huo bado hakujatumwa kikosi kikubwa cha maafisa wa usaidizi.

MSF linasema kumekuwa na ongezeko kubwa katika mji mkuu wa Guinea, Conakry, ongezeko linaloondosha matumaini kwamba maambukizi ya Ebola yanadhibitiwa .

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Mkuu wa shirika la Marekani la kupambana na magonjwa Thomas Frieden

Rais wa Guinea, Alpha Conde, anasema anaamini iwapo mlipuko huo ungeingiliwa kati na mapema ingezuia janga lililopo.

Rais Conde anasema nchi yake inahitaji mambo kadhaa ili kuimarisha vita dhidi ya Ebola.

Kwingineko nchini Uhispania, watu 7 zaidi wamo katika uangalizi hospitalini kuona iwapo wameathirika na Ebola.

Image caption Madaktari kadhaa kutoka Tanzania wameenda Siera Leone kusaidia katika vita dhidi ya ugonjwa huo hatari

Miongoni mwao ni wafanyakazi wawili wa biashara ya ususi na urembo wa nywele waliomkaribia muuguzi aliyeathiriwa na ugonjwa huo.

Kwa sasa ni yuko katika hali mahututi, na anaarifiwa yumo katika hatari ya kufariki.

La kutia moyo ni kuwa muuguzi mmoja nchini Austarlia aliwekwa kwenye karantini na kufanyiwa uchunguzi wa maabara amegunduliwa hana Ebola.

Waziri wa usalama wa ndani Marekani, Jeh Johnson amesema anataka nchi zaidi kuidhinisha ukaguzi wa virusi hivyo katika viwanja vya ndege vya kimataifa kuzuia kuenea kwake.