USA:Yaahidi dola millioni 212 Gaza

Haki miliki ya picha Getty
Image caption John Kerry Katikati na viongozi wa mataifa ya kiarabu

Marekani imeahidi dola millioni 212 za msaada ili kusaidia kulijenga eneo la Gaza katika mkutano wa kuomba msaada mjini Cairo.

Utawala wa Palestina unaomba dola bilioni 4 kulijenga eneo la Gaza baada ya siku hamsini za mapigano kati ya Israel na Hamas.

Takriban raia laki moja wa Gaza walipoteza makaazi yao katika vita huku miundo msingi pia ikiharibiwa.

Awali marais wa Palestina na Misri waliitaka Israel kudumisha amani ya mda mrefu.

Waliitaka Israel kuikabidhi Palestina ardhi walioiteka katika vita vya mwaka 1967 na kukubali suluhu kwa wakimbizi wa Palestina ili Israel Kutambulika.

Mgogoro huo wa wiki saba katika eneo la Gaza ambao uliisha baada ya makubaliano mnamo tarehe 26 Agosti,ulisababisha mauaji ya Wapalestina 2100 wengi wao wakiwa raia ,wanajeshi 67 wa Israel pamoja na raia sita wa taifa hilo kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa.

Waziri wa maswala ya kigeni nchini Marekani John kerry amesema kuwa huku msimu wa baridi ukikaribia ,maelfu ya raia wa Palestina walioachwa bila makao wanahitaji usaidizi wa haraka.