Kiongozi wa waasi ashambuliwa Ukraine

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Kiongozi wa waasi Ukraine Mashariki Pavel Gubarev

Mwanasiasa anayetambulika kama muasi mkuu nchini Ukraine Pavel Gubarev, yuko katika hali mahututi hospitalini baada ya watu waliokuwa wamejihami kumpiga risasi akiwa ndani ya gari lake.

Taarifa zinasema kuwa gari hilo liligonga mlingoti na hapo ndipo alipojeruhiwa.

Duru zinasema kuwa gari la bwana Pavel Gubarev ambaye anaongoza vuguvugu linaloungwa mkono na Urusi, lilishambuliwa katika eneo la Donetsk akiwa anaelekea Rostov-on-Don nchini Urusi.

Kwa sasa amelazwa hospitalini mjini Rostov.

Duru zinasema waasi wenzake aliokuwa nao waliponea.

Waasi wanadhibiti sehemu kubwa ya eneo hilo.

Mkewe kiongozi huyo wa waasi alinukuliwa akisema mumewe hakupata jeraha lolote la risasi na kwamba majeraha yake yalitokana na gari lake kugonga mlingoti.

Mnamo mwezi Februari, Bwana Gubarev aliongoza harakati za kuudhibiti eneo la Donetsk zilizofanywa na mamia ya waasi wanaoungwa mkono na Urusi.

Wanaharakati hao walitangaza eneo la Donetsk kuwa eneo huru na hata kupewa wadhifa wa gavana.

Mnamo mwezi Aprili, makabiliano mapya yakazuka tena kati ya waasi hao na wanajeshi wa serikali ya Ukraine.

Kwa sasa makubaliano ya kusitisha vita yaliyofikiwa tarehe 5 Septemba bado yanatekelezwa lakini makabiliano ya mara kwa mara yamekuwa yakiripotiwa katika baadhi ya maeneo hasa eneo linalozunguka uwanja wa ndege wa Donetsk.