Muuguzi mwingine ana Ebola Marekani

Haki miliki ya picha Getty

Muguzi mwingine wa afya mwenye umri wa miaka 26 nchini Marekani amepatikana na ugonjwa wa Ebola katika jimbo la Texas.

Maafisa wa afya wanasema muuguzi huyo tayari anapokea matibabu baada ya kuambukizwa ugonjwa huo na mwanamume raia wa Liberia aliyefariki kutokana na ugonjwa huo wiki jana.

Maafisa nchini Marekani wanasema wanawachunguza watu wengine 48 waliokaribiana na raia mgonjwa aliyefariki na Ebola wakiwemo wahudumu wa afya waliomtibu.

Shirika la afya duniani linasema watu 4,447 wamefariki na Ebola, hasa katika mataifa ya Afrika Magharibi.

Nina Pham alimtibu raia wa Liberia aliyekuwa mtu wa kwanza kuugua Ebola nchini Marekani Thomas Duncan. Alifariki akipokea matibabu.

Madaktari walisema kuwa muuguzi huyo yuko katika hali nzuri tangu Jumanne.

Muuguzi wa pili kuambukizwa Ebola hajatajwa , hata hivyo inaarifiwa pia alimhudumia bwana Duncan alipokuwa hospitalini.

Aliwekwa karantini mara moja baada ya kuonyesha dalili za ugonjwa wa Ebola.