Boko Haram lakiuka 'mkataba' na serikali

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Boko haram

Ripoti kutoka nchini Nigeria zinasema kuwa watu wanaokisiwa kuwa wanamgambo wa Boko Haram wamewaua watu kadha kwenye jimbo la Borno siku moja tu baada ya jeshi la Nigeria kusema kuwa limeafikia makubaliano ya kusitisha vita na kundi hilo.

Katika shambulizi moja wanamgambo hao wanaripotiwa kuwaua watu mashuhuri katika kijiji cha Abadam kazkazini mwa jimbo hilo na kuwalazimu watu wengine wengi kukimbilia nchi jirani ya Niger.

Utawala nchini Nigeria umesema kuwa mashambulizi hayo dhidi ya vijiji vitano kwenye jimbo la Borno huenda yalitekelezwa na makundi mengine ya wahuni.

Siku ya Ijumaa jesh la Nigeria lilisema kuwa maafikiano ya kusitisha vita na Boko Haram yatahusu kuachiliwa kwa wasichana zaidi ya 200 waliotekwa na wanamgambo hao miezi sita iliyopita.