Gereza lavamiwa Kivu Kaskazini

Mwanajeshi wa DRC atazama gari lao liloshambuliwa Kivu Kaskazini Haki miliki ya picha Reuters

Watu waliokuwa na silaha wamevamia gereza mashariki mwa Jamhuri ya Demokrasi ya Congo na kuwaachilia huru wafungwa kama 400.

Uvamizi huo ulitokea Jumamosi usiku katika mji wa Butembo katika jimbo la Kivu Kaskazini.

Msemaji wa serikali ya Congo, Lambert Mende, alithibitisha kuwa gereza ilivamiwa lakini aliiambia BBC kwamba bado wanachunguza vipi shambulio hilo lilifanywa.

Kumetokea mashambulio katika jimbo la Kivu Kaskazini katika siku 10 zilizopita - mashambulio yanayodaiwa kufanywa na wapiganaji wa ADF kutoka Uganda.

Huku nyuma, afisa wa haki za kibinaadamu wa Umoja wa Mataifa amelaani hatua ya Jamhuri ya Demokrasi ya congo kumfukuza nchini mwakilishi wao. Scott Campbell alitangazwa Alkhamisi kuwa hatakiwi kuwepo nchini DRC.

Katika taarifa yake mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na haki za kibinaadamu, Zeid Raad al-Hussein, alisema wafanyakazi wengine wawili wa Umoja wa Mataifa piya wametishwa vikali.

Kufukuzwa kwa Scott Campbell kulitangazwa siku moja baada ya ripoti ya Umoja wa Mataifa kutuhumu kuwa polisi wa Congo wanafanya vitendo vinavyokiuka sana haki za kibinaadamu.