Man United yakwaa kisiki

Haki miliki ya picha AFP

Ligi kuu ya England imeendelea jana usiku ambapo Manchester United ilijikuta ikibanwa mbavu na kushindwa kufurukuta ugenini kwa Westbromwich Albion na kutoka sare ya mabao 2-2 licha kwamba ilitawala mchezo huo.

Mchezo huo wa pekee kwa ratiba ya ligi hiyo ulishuhudiwa Man United ikishindwa kupata walau ushindi wake wa kwanza nje ya uwanja wake wa nyumbani tangu timu hiyo iwe chini ya kocha Louis Van Gaal.

Ni bao la Daley Blind katika dakika za mwisho za mchezo ambalo limeiokoa Manchester United kuzama katika mpambano huo. Awali Stephane Sessegnon wa Westbrom aliitungua United kwa bao la mapema kabla ya Marouane Fellaini aliyeingia kipindi cha pili kusawazisha muda mfupi tu baada ya kuingia uwanjani.

Mshambuliaji kijana Saido Berahino aliipatia Westbrom goli la pili ambalo lilidumu hadi pale Blind aliposawazisha na kuinusuru United na kichapo katika mtanange huo uliochezeshwa na mwamuzi Mike Dean.