Kupotea wanafunzi Mexico: Meya atafutwa

Image caption Picha za wanafunzi waliopotea katika mji wa Iguala nchini Mexico.

Mwendesha mashtaka mkuu wa serikali ya Mexico amesema Meya Jose Luis Abarca aliamuru polisi kufanya operesheni, ya kuwazuia wanafunzi kutovuruga shughuli iliyokuwa imeandaliwa na mke wake.

Wana ndoa hao wanasemekana wamejificha.

Kwa mara ya mwisho wanafunzi hao walionekana wakiwa wamekusanywa katika magari ya polisi baada ya mapigano kati yao na polisi Septemba 26.

Mwanasheria Mkuu wa serikali Jesus Murillo Karam amesema Bwana Abarca, mke wake Maria de los Angeles Pineda na mkuu wa polisi Felipe Flores wanatafutwa"kama watu binafsi ambao waliandaa shughuli ambayo ilifanyika Iguala, Septemba 26".

Image caption Ukumbi wa mji wa Iguala ukiwa umechomwa moto na wanaandamanaji wanaopinga kupotea kwa wanafunzi

Pia amemshutumu Bi Pineda kuwa alikuwa na uhusiano na genge la kuuza dawa za kulevya la Guerreros Unidos (United Warriors), lililo katika eneo hilo.

Maafisa wa polisi wa manispaa wamekamatwa kuhusiana na mapigano hayo waliporipotiwa kukiri kuwakamata na kuwakabidhi wanafunzi kwa genge hilo.

Kiongozi wake anayeshukiwa, Sidronio Casarrubias, alikamatwa wiki iliyopita.

Waandamanaji wanaopinga kupotea kwa wanafunzi hao wamechoma moto ukumbi wa manispaa hiyo siku ya Jumatano.

Kazi ya kuwatafuta wanafunzi inaendelea, kwa maafisa wa polisi kutafuta kila mahali katika eneo la Iguala yakiwemo machimbo na visima.

Pia kuna maandamano katika miji na majiji ya Mexico.

Utafutaji unaendelea:

Image caption Polisi wakitafuta miili ya wanafunzi waliopotea ndani na kuzunguka mji wa Iguala

Wanafunzi walisafiri hadi Iguala kupinga kupotea kwa wanafunzi wenzao na wamechanga fedha kwa ajili ya chuo chao ili kufanikisha kazi ya kuwapata wenzao.

Polisi waliyafyatulia risasi mabasi yao wakati wakirejea katika mji wao wa Ayotzinapa. Watu sita watatu kati yao wanafunzi waliuawa kufuatia shambulio hilo.

Wanafunzi 43 walithibitika kutoweka katika siku zilizofuata.

Kugunduliwa kwa makaburi mengi ya pamoja katika mji wa Iguala kumezusha wasiwasi juu ya hatima ya wanafunzi waliopotea.

Lakini matokeo ya kipimo cha DNA yameonyesha kuwa hawakuwa miongoni mwa miili 30 iliyofanyiwa uchunguzi mpaka sasa. Miili hiyo bado haijatambuliwa.

Serikali ya Mexico imetoa zawadi ya peso milioni 1.5 sawa na dola za Kimarekani $110,000, au pauni za Kiingereza£68,000 kwa mtu atakayetoa taarifa zitakazowezesha kujua walipo wanafunzi hao.

Zaidi ya polisi wa Mexico 1,200 wamesambazwa katika eneo la Iguala na kuzunguka ili kuwatafuta wanafunzi waliopotea.