Chama tawala chashinda uchaguzi Botswana

Image caption Rais Khama

Tume ya uchaguzi nchini Botswana inasema kuwa chama tawala nchini humo kimeshinda uchaguzi mkuu uliondaliwa siku ya ijumaa.

Hata kama bado shughuli ya kuhesabu kura inaendelea tume hiyo imetangaza kupitia kwa akaunti yake ya Twitter kuwa chama cha BDP kikiongozwa na rais Ian Khama kilishinda viti 33 kati ya viti 57 vya bunge.

Chama kinahitaji viti 29 ili kuchukua madaraka. Chama pinzani cha Umbrella for Democratic Change kilipata viti 14.

Wabunge wengine wanne kati ya wale 64 watachaguliwa na bunge jipya huku rais na mkuu wa sheria akijaza viti vyengine viwili vilivyosalia.

Matokeo ya awali katika uchaguzi wa mabaraza yalionyesha kazi nzuri iliofanywa na vyama viwili vya upinzani katika maeneo ya miji ya Botswana ikiwemo mji mkuu wa Gaberone.

Baada ya kuchaguliwa wabunge hao watamchagua kiongozi.Rais Khama mwana wa rais wa kwanza wa taifa hilo ana uwezekano mkubwa wa kushinda hatamu ya pili.