Kijana akataa kula kwa mwaka mmoja

Image caption Landon

Landon Jones mwenye umri wa miaka 12 ni kijana aliyepoteza hamu ya kula pamoja na ile ya kunywa kwa mwaka mmoja kufikia sasa nchini Uingereza.

Mnamo mwezi Octoba mwaka uliopita kijana huyo aliamka akiwa hana hamu ya kula wala kunywa.

Landon ambaye alikuwa kijana mwenye nguvu aliyependa kukimbia,kupeleka baisklei pamoja na kucheza na marafiki zake.

Madaktari katika hospitali tano tofauti wameshindwa kubaini ni nini kinachomsumbua kijana huyo.

Wazazi wake Michael na Debbie wametafuta tiba kwa udi na uvumba lakini majaribio yote ya matibabu yameshindwa kufaulu.

Wataalam wanaamini kwamba Landon ni kijana aliye na ugonjwa wa kipekee ulimwenguni.

Katika kipindi cha mwaka mmoja kijana huyo amepoteza kilo nyingi za mwili wake .

Wazazi wake wamejaribu kila wawezalo kumshawishi mwana wao kula ,lakini ni nadra kwa kijana huyo wa miaka 12 kutia chochote mdomoni.

Vile vile katika kipindi cha mwaka mmoja amekosa masomo kwa takriban siku 65 mbali na kuwa wazazi wake wanasema kwamba hajakimbia kwa miezi kadhaa sasa,huku akilazimika kuwaangalia rafikize kutoka dirisha la nyumbani.