Habari za BBC ndani ya Tigo

Image caption Mkuu wa huduma za internet wa Tigo Tanzania, David Zacharia (kulia) akiongea wakati wa uzinduzi wa internet.org jijini Dar Es Salaam. Kushoto ni Naheed Hirji, Mkuu wa ukuzaji huduma za Facebook Afrika Mashariki na Kusini. Picha na Khalfan Said.

Uwapo Tanzania unaweza kusoma habari kutoka tovuti ya BBC bure hata kama simu haina fedha.

Ni sehemu ya mpango mpya uliozunduliwa kati ya mtandao wa kijamii wa Facebook kutoka Marekani na Tigo, inayotoa huduma za simu Kampuni hizo mbili zimezindua huduma ijulikanayo kama internet.org ambayo inawawezesha wateja wa Tigo kutumia baadhi ya tovuti bila gharama.

Internet.org ni mpango wa kimataifa unaoyashirikisha miongoni mwa makampuni makubwa ya teknolojia, taasisi zisizo za kibiashara zinazofanya kazi pamoja kufikisha huduma ya internet kwa mabilioni ya watu duniani ambao hawapati huduma ya internet.

Kampuni ya mtandao wa kijamii ya Facebook yenye makao yake nchini Marekani ni waanzilishi wa internet.org.

Mkuu wa ukuzaji wa huduma za Facebook, Afrika Mashariki na Kusini, Naheed Hirji ameileza BBC kuwa soko la Kiswahili linakua na kwamba kampuni yake imeona Tanzania kuna fursa ya kuwafikia watu wengi.

"Tunazindua huduma hii Tanzania kwasababu kutokana na utafiti wetu tuliofanya, chini ya asilimia 20 ya watu wanapata huduma ya interenet.

Kwa hiyo tumeona kuna fursa kubwa na nafasi ya kusaidia kuwaunganisha watu hawa kupata huduma za internet", alieleza Hirji.

Akafanua kuwa: "Lugha ya Kiswahili ni muhimu sana kwetu, takriban mwaka mmoja uliopita tulitafsiri Facebook yote ipatikane kwa lugha ya Kiswahili , si tu kwa watumiaji wa Tanzania.

Kwa hiyo tulitafsiri Facebook yote ipatikane kwa Kiswahili ili iweze kuwawekea mazingira mazuri na kuwafikia wengi zaidi".

Taarifa ya hivi karibuni kutoka mamlaka ya mawasiliano Tanzania - TCRA, ilionyesha kuwa idadi ya watu wanaotumia internet iliongezeka kutoka milioni saba na nusu mwaka 2012 mpaka kufikia milioni tisa nukta tatu mwaka huu 2014.

Katika uzinduzi kuna tovuti zisizopungua 15 za makampuni ya ndani na nje ya Tanzania ambazo huduma zao zitakuwa zikipatikana bure kwa wateja wa Tigo, ikiwemo BBC kwa lugha ya Kiingereza na Kiswahili, vile vile tovuti ya Mwananchi.

Kampuni ya Tigo imesema inakusudia kufanya huduma kuwa endelevu na kuongeza nyingine kadri muda unavyosonga mbele.

Mkuu wa huduma za internet na vifaa vinavyotumia internet katika Tigo, David Zacharia ameileza BBC.

Hata hivyo wachambuzi wa maswala ya teknolojia wanasema lengo la kuchochea na kuwafikishia watu wengi zaidi huduma ya internet bado litakutana na ugumu mwingine hasa kutokana na gharama za kununulia simu zenye uwezo wa kutumia internet kuwa kubwa na upatinaji wa umeme wa uhakika katika baadhi ya maeneo ya vijijini, japokuwa umeme wa jua umeanza kutumika kwa wingi.