Rais Michael Sata wa Zambia aaga dunia

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Rais Michael Sata wa Zambia afariki dunia

Familia ya Bwana Sata wameiambia BBC kuwa Rais wa Zambia, Michael Sata, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 77 katika hospitali ya London alikokuwa akitibiwa ugonjwa ambao haujatajwa.

Kifo chake kimetokea siku chache baada ya Zambia kusherehekea miaka 50 ya uhuru wa nchi hiyo.

Mwanasiasa huyo mkongwe aliingia madarakani mwezi Septemba 2011 baada ya kuongoza chama chake cha Patriotic Front, na kumshinda Rupiah Banda, ambaye alikuwa rais wakati huo na chama chake cha Movement for Multi-Party Democracy, kikiwa madarakani kwa miaka ishirini.

Michael Chilufya Sata alizaliwa mwaka 1937 katika mji wa Mpika, eneo ambalo lilikuwa wakati huo ni Northern Rhodesia. Muumini wa dini ya Kikristo ya madhehebu ya Katoliki, alifanya kazi kama afisa polisi, mfanyakazi wa reli na mwanachama wa chama cha wafanyakazi wakati wa utawala wa kikoloni. Baada ya Zambia kupata uhuru wake, pia aliishi kipindi fulani mjini London, akiwa mfanyakazi wa reli, na kurejea Zambia, akiwa na kampuni ya teksi.

Akiwa mwenye sauti ya mkwaruzo yakiwa ni matokeo ya kuvuta sigara kwa muda mrefu, Bwana Sata aliibuka katika siasa na kupata umaarufu katika miaka ya 1980.

Haraka akapata sifa ya kuwa gavana mwenye kuchapa kazi kwa bidii, wakati akiongoza jimbo la Lusaka na mtu wa utekelezaji kwa vitendo.

Lakini pia alijulikana kama mtu wa kutoa amri, mtu asiyeendekeza urafiki na mkali- na wapinzani wake walisema jina alilopewa la bandia la "King Cobra" alikuwa anastahili kuitwa hivyo.

Kwa mara ya kwanza alionekana kama mtu ambaye angetekeleza ahadi za kupambana na rushwa na kupata ufumbuzi wa tatizo la ajira na kuleta ustawi wa jamii. Lakini kipindi chake madarakani kiligubikwa na kuuzima upinzani wa kisiasa na kudorora kwa uchumi.

Bwana Sata ni rais wa pili wa Zambia kufariki dunia akiwa madarakani.