Ebola Marekani:Muuguzi apinga karantini

Haki miliki ya picha
Image caption Bi Kaci Hickox akiwekwa chini ya karantini katika jimbo la New Jersy, Marekani baada ya kurejea kutoka Sierra Leone, alikokuwa akiwahudumia wagonjwa wa Ebola

Muuguzi wa Marekani, ambaye alikuwa akihudumia wagonjwa wa Ebola nchini Sierra Leone, ameamua kupambana na utawala wa jimbo la Maine, akihoji haki yake ya kuwekwa chini ya karantini.

Kaci Hickox anasisitiza, "Ni mzima kabisa, unaweza kunikumbatia" na anasema"si lengo lake kuhatarisha afya ya mtu yeyote".

Hata hivyo anafikiri kumweka mtu chini ya karantini haikubaliki na ni jambo linalokosa uahlisia wa kisayansi.

Bi Hickox ametangaza nia yake ya kupinga uamuzi wa jimbo la Maine la kuwawekea watu karantini na ikilazimu atakwenda mahakamani kupinga hatua ya jimbo la Maine.

Kwa upande wao wanasayansi wanaoshauri Serikali kuu juu ya Ebola wanasema kuwa hakuna haja ya kutumia karantini kama hatua ya kuzuia ugonjwa huo kusambaa.

Haki miliki ya picha
Image caption Nyumba anayoishi Kaci Hickox, huko Maine, muuguzi aliyewahudumia wagonjwa wa Ebola, Afrika Magharibi 2014.

Hata hivyo maafisa wa afya wa jimbo lake la Maine wametishia kwenda mahakamani kupata idhini ya kuwatumia wanajeshi kuhakikisha haondoki nyumbani kwake.

Bi Hickox amesema alijisikia kama mhalifu baada ya kuwekewa karantini huko Newark aliporejea kutoka Sierra Leone Ijumaa iliyopita.

Aliachiliwa Jumatatu na kusafirishwa kwenda nyumbani kwake Maine.

Idara ya afya ya jimbo la New Jersey imesema Bi Hickox hakupatikana na maambukizi ya Ebola baada ya kupimwa Jumamosi na hakuwa na dalili za Ebola kwa saa 24.

Gavana wa New Jersey Chris Christie ametetea hatua za jimbo lake za kuweka karantini na amesema kuwa Bi Hickox aliwasili Marekani akiwa na joto la homa - jambo ambalo muuguzi huyo analikanusha.