Mume mgomvi aandaliwa mlo wa kondomu

Image caption kondomu

Mwanamke mmoja mwenye watoto watatu katika wilaya ya Kole nchini Uganda alimuandalia mumewe mlo wa mipira ya kondomu kufuatia ugomvi usiokwisha kati yao.

Mwanamke huyo ambaye ni mkaazi wa eneo la Arao aliripotiwa kununua paketi tatu za kondomu aina ya "Trust" kutoka duka jirani kabla ya kuzipika na kumuandalia mumewe kama chakula baada ya kurudi nyumbani akiwa amelewa chakari.

Kwa mujibu wa gazeti la Daily Monitor la nchini Uganda, mwanamke huyo aliikata kata mipira hiyo ya kondomu ambayo ilikuwa haijatumika katika vipande vidogo vidogo na kuvichemsha kwa muda kabla ya kuvikaanga kwa mafuta ya kupikia na viungo vingine.

Wakati mumewe alipowasili kutoka kubugia pombe katika eneo jirani la kibiashara la Odede,aliandaliwa mlo huo katika sahani tofauti moja ikiwa na mipira hiyo kama mboga na nyingine ikiwa na mkaa.

Lakini jamaa huyo alibaini njama za mkewe baada ya kuonja mlo huo na kugundua ulikuwa na ladha tofauti.

Hatua hiyo ilikuwa ikilenga kumfunza mume huyo ambaye amedaiwa kuzua ugomvi na mkewe kila anapolewa na kurudi nyumbani.