Kukatika kwa umeme Bangladesh gizani

Image caption Njia ya umeme wa msongo mkubwa Bangladesh

Bangladesh imekumbwa na tatizo kubwa la ukosefu wa umeme baada ya njia ya umeme inayounganisha nchi hiyo na umeme wa gridi ya taifa kutoka India kukatika.

Kukatika kwa umeme kulianza saa za mchana kwa saa za Bangladesh na kuathiri maeneo yote ya nchi hiyo yanayounganishwa na umeme wa gridi ya taifa.

Maafisa wamesema wahandisi wanafanyakazi ya kurekebisha tatizo hilo, ambalo chanzo chake bado hakijafahamika.

Image caption Ramani ya Bangladesh

Bangladesh ilianza kununua umeme kutoka India mwezi Oktoba mwaka jana.

Mkuu wa umeme wa gridi ya taifa nchini Bangladesh, Chowdhury Alamgir Hossain, ameliambia gazeti la Dhaka Tribune kwamba kukatika kwa umeme kulianza baada ya kutokea hitilafu katika kituo kidogo cha kusambaza uememe unaotoka India.

Hali hiyo ilisababisha mitambo mingine ya umeme nchini Bangladesh kuzimika mmoja baada ya mwingine, amesema Bwana Hossain.

Maafisa kutoka Bodi ya Maendeleo ya Umeme wameliambia gazeti la Daily Star nchini Bangladesh kuwa wanatarajia kurejesha hali ya kawaida ya umeme ifikapo saa tisa alasiri kwa saa za huko.

Njia ya umeme mkubwa inatoka Baharampur Bengal Magharibi kwenda Bheramara katika wilaya ya Kushtia, kusini magharibi mwa Bangladesh.