Kanisa lawatimua waumini walio nusu uchi

Haki miliki ya picha AP
Image caption Waumini waliovalia nguo fupi watimuliwa kanisani

Waumini wa kanisa katoliki la St. Francis mjini Diani kusini mwa pwani ya Kenya walipigwa na butwaa baada ya baadhi yao kuzuiwa kuingia katika kanisa hilo kutokana na mavazi yao yaliokuwa nusu uchi.

Julia baraza ambaye alikuwa amevalia kisibao ,ukanda wa manjano na viatu vyenye kisigino kirefu alishangazwa na sheria hizo mpya ambazo zilimsababisha kukosa misa ya asaubuhi.

Kulingana na gazeti la the standard nchini kenya,Julia alisema kuwa watu wawili walimsimamisha nje ya mlango wa kanisa hilo na kumwambia kwamba mtindo wake wa mavazi ulipigwa marufuku katika kanisa hilo na kwamba ametakiwa kuvaa mavazi ya heshima.

Aidha wasichana waliokuwa wamevalia suruali walilazimishwa kujifunga leso juu yake.

Julia alisema kwamba iwapo makanisa yataanza kufuata sheria kama hizo basi wengi hawatahudhuria maombi.

Baadhi ya waumini wamesema kuwa mhubiri wa kanisa hilo aliyejulikana kama Joseph pekee alikuwa ametangaza katika ibada ya awali kwamba mavazi yasio ya heshima hayatakubalika katika kanisa hilo.