Takriban watu 24 wafa maji Uturuki

Image caption Kikosi cha uokoaji kikiwa na miili ya waliopoteza maisha

Takriban watu 24 wamepoteza maisha na wengine wengi hawajulikani walipo baada ya Boti inayoelezwa kubeba wahamiaji kuzama baharini mjini Istanbul nchini Uturuki

Ajali hiyo imetokea katika eneo bahari Nyeusi na bahari ya Marmara zinapokutana.

Operesheni ya uokoaji angani, baharini na chini ya bahari inaendelea miili mingi ikiripotiwa kuibuliwa kutoka majini.

Operesheni ya baharini ina changamoto ya kuwepo kwa upepo mkali , mmoja wa waokoaji Ali Saruhan amesema Boti hiyo ni ndogo lakini ilibeba watu 40 akieleza kuwa ameshuhudia miili ya watoto ikielea baharini.

Uraia wa wahamiaji hao bado haujajulikana, vyombo vya habari vinasema ni aghalab kwa chombo kilichobeba wahamiaji kuwa katika eneo hilo.

Mwandishi wa BBC anasema Uturuki ni moja ya vituo vikuu kwa wahamiaji wanaosafiri kwenda nchi za ulaya, lakini wengi wao husafiri kupita bahari ya Aegean mpaka Ugiriki.

Boti zinazowasafirisha wahamiaji hao hujaza wasafiri kupita uwezo wake, huku wahamiaji hao wakilipa nauli ya maelfu ya dola kwa ajili ya kusafirishwa.

Miezi miwili iliyopita kundi la wahamiaji, wengi wao raia wa Syria na Afghanistan waliokolewa eneo la kaskazini mwa pwani ya Bahari mjini Istanbul wakiripotiwa kwenda nchi za ulaya.