Merkel:Ni sawa Uingereza kujitoa EU

Image caption Kiongozi wa Ujerumani Angela Merkel akiteta jambo na Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron

Kiongozi wa Ujerumani, Angela Merkel amesema yuko tayari kuona Uingereza ikijitoa kutoka Umoja wa UIaya kuliko kukwamisha uhuru wa watu kuhama na kutafuta ajira miongoni mwa nchi wanachama, kwa mujibu wa jarida la Der Spiegel la Ujerumani.

Bi Merkel inadaiwa anahofia kwamba Uingereza inakaribia hatua ambayo haitakuwa rahisi kubakia ndani ya umoja huo.

Ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza ya Downing Street haikuwa tayari kuzungumzia swala hilo.

Waziri Mkuu wa Uingereza, Bw Cameron anataka kujadiliana vipengele vya uanachama wa Uingereza kabla ya kufanya kura ya maoni ya kutaka kuendelea au kujitoa katika Umoja wa Ulaya.

Waziri huyo mkuu alisema uhuru wa watu kuhamia nchi nyingine kutafuta ajira ni jambo atakalolipa kipaumbele katika mkakati wake wa mahusiano na nchi za Ulaya, lakini Bi Merkel ameelezewa na jarida hilo kusema atasitisha kuunga mkono uanachama wa Uingereza katika EU endapo Cameron ataendelea kuhamasisha mageuzi ya sera za uhamiaji.