Mitandao kutumiwa kumaliza migomo Kenya

Haki miliki ya picha PA
Image caption Mitandao ya facebook na twitter

Wasimamizi wa vyuo vikuu nchini Kenya wameagizwa kufungua mitandao ya Twitter na facebook ambayo wanafunzi watatumia kutoa malalamishi yao kwa lengo la kuzuia machafuko katika taasisi hizo.

Waziri wa Elimu nchini Kenya Jacob Kaimenyi amesema kuwa vifaa hivyo vya mawasiliano vitawasaidia wanafunzi kutoa malalamishi yao mbali na kupata majibu kutoka kwa wasimamizi.

Profesa Kaimenyi amesema kuwa vyuo vikuu vimeshindwa kuchukua fursa ya teknolojia ili kuwasiliana zaidi na wanafunzi hao.

''Kuna umuhimu wa kuwepo kwa mfumo ulio wazi wa mawasiliano na mitandao ya kijamii ni muhimu sana.

Ndio maana tunaviambia vyuo vikuu kufungua mitandao ya twitter na ile ya facebook ambapo wataweza kuwasailiana na wanafunzi'',alisema katika mkutano wa elimu.

Waziri huyo ameshtumu mbinu zinazotumiwa na vyuo vikuu kukandamiza upinzani mbali na kudhibiti maswala ya wanafunzi kama vile uchaguzi wao na kuwasingizia katika maswala ya utovu wa nidhamu bila kuwasikiza.