Mfuko wa kupambana na Ebola waanzishwa

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Dlamini Zuma

Viongozi wa juu wa maswala ya biashara barani Afrika wameanzisha mfuko wa kusaidia nchi zilizoathiriwa na ugonjwa wa Ebola.

Kiasi cha dola milioni 28.5 zilipatikana katika mkutano wa harambee mjini Addis Ababa nchini Ethiopia kwa ajili ya kuwapeleka wahudumu wa afya nchini Guinea, Sierra Leone na Liberia.

Wataalam wanasema kama wanataka kukabili ugonjwa huu kwa kasi hakuna budi kuanza na nchi hizo tatu.

Takriban watu 5000 kati ya 14,000 wamepoteza maisha kutokana na Virusi vya ugonjwa huu hasa nchini Liberia.

Akiongea baada ya mkutano wa Addis Ababa, mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Dlamini Zuma amesema rasilimali zilizokusanywa zitakua sehemu ya mchakato wa kupambana na ugonjwa huo siku za usoni.

mkutano wa Addis Ababa umefanyika wakati Liberia ilipotangazwa na Shirika la madaktari wasio na mipaka,MSF kuwa imefanikiwa kupunguza idadi ya maambukizo mapya.

Hata hivyo shirika hilo limesema bado Ebola iko kwa kiasi kikubwa nchini Guinea na Sierra Leone.