Afueni kwa wanablogu Ethiopia

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Wanablogu wa zone 9 waponea kufutiwa kosa moja

Mahakama moja nchini Ethiopia imewaagiza waendesha mashtaka kutupilia mbali shtaka moja dhidi ya waandishi habari na wanablogu tisa waliokamatwa nchini humo miezi sita iliyopita.

Tisa hao walikamatwa mwezi Aprili huku wa kumi akishtakiwa akiwa nje ya nchi. Kesi yao sasa imeahirishwa hadi mwezi ujao.

Hii ilikuwa mara ya kumi na mbili kwa washukiwa hao wanaojulikana kama wanablogu wa Zone 9, kufikishwa mahakamani.

Jaji mpya katika kesi hiyo aliwaagiza viongozi wa mashtaka kutupilia mbali shtaka la uchochezi.

Pia aliitaka serikali kufanyia marekebisho shtaka la pili linalohusiana na ugaidi, akitaka ufafanuzi zaidi kuhusu vipi wanablogu hao walishirikiana na kundi lililopigwa marufuku la Ginbot 7.

Hata hivyo wote tisa wamekanusha mashtaka hayo ya kupokea ufadhili kutoka kwa shirika la Ginbot 7 ambalo lina makao yake Marekani.

Katika kikao cha leo, wawili wa washukiwa hao walidai kuteswa na maafisa wa polisi katika kizuizi.

Ethiopia imekashifiwa mara kwa mara na mashirika ya kutetea haki za kibinadamu kwa rekodi yake ya kuwafunga wapinzani na waandishi wa habari.

Mwezi Uliopita, Marekani ilielezea wasiwasi kuhusu kufungwa gerezani kwa mwanahabari Temesegn Desalegn baada ya kupatikana na hatia ya kuchapisha habari za uchochezi mwaka wa 2012.